Rais William Ruto amesema Serikali inaimarisha operesheni za usalama katika kaunti ya Turkana na viunga vyake ili kukabiliana na wizi wa mifugo.
Rais alisema Serikali itapeleka Polisi wa Kitaifa wa akiba, kusaidia askari polisi kusimamia usalama wa eneo hilo.
Aliongeza kuwa kaunti ndogo tatu mpya za Suguta, Lokiriama na Aroo zitabuniwa na kuanza kufanya kazi ndani ya siku 90.
“Hatuwezi kuruhusu watu wachache kusababisha ukosefu wa usalama na kuharibu ajenda yetu ya maendeleo,” alisema.
Alisema hayo siku ya Alhamisi wakati wa Tamasha la Utamaduni na Utalii la Turkana (Tobong’u Lore) mjini Lodwar, Kaunti ya Turkana.
Hafla hiyo ya kila mwaka ilileta pamoja watu wa jamii hiyo kutoka Sudan Kusini, Uganda na Ethiopia.
Waliohudhuria ni Mawaziri Alfred Mutua na Aisha Jumwa, Magavana Jeremiah Lomorukai (Turkana), Jonathan Bii (Uasin Gishu) na Mohammud Ali (Marsabit), na Wabunge na Wawakilishi wa Wadi wenyeji.