Rais Ruto, Raila wakutana Ikulu ya Mombasa

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akiwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga

Rais William Ruto leo Jumatatu amekuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga. 

Mkutano kati yao umefanyika katika Ikulu ya Mombasa na kuhudhuriwa na Naibu Rais Prof Kithure Kindiki na kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah miongoni mwa viongozi wengine.

Hii ni mara ya kwanza kwa Raila kujitokeza hadharani nchini baada ya kubwagwa katika kinyang’anyiro cha kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) katika uchaguzi uliofanyika Februari 15, 2025 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti ndiye aliyeibuka mshindi wa uchaguzi huo.

Rais Ruto alikuwa mstari wa mbele kumnadi Raila kwa viongozi wa nchi za bara la Afrika, akimsifia kama mtu aliye na ujuzi na tajiriba ya kipekee ya kuliongoza bara la Afrika kwenye wadhifa huo.

Kwa upande wake, Raila alifanya kampeni kali akitembelea mataifa takriban 49 barani humo kutafuta uungwaji mkono.

Ila, licha ya juhudi zao, Raila alitemwa na Youssouf ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Djobouti katika hatua iliyowagawanya Wakenya.

Kunao waliosherehekea ushinde wa Raila huku wengine wakiuomboleza.

Katika Ikulu ya Mombasa, Raila amesema atatafuta ushauri wa chama chake cha ODM juu ya mwelekeo wa kuchukua baada ya kushindwa kwenye kinyang’anyiro cha AUC.

Raila amesema “yuko tayari kufanya kazi na wengineo kwa ajili ya umoja wa taifa”.

Katika chama chake cha ODM, migawanyiko imeshamiri huku mrengo mmoja ukiunga mkono serikali ya Kenya Kwanza kwa dhati na mwingine ukiikosa vikali.

Hususan, Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna ambaye pia ni Seneta wa Nairobi ameibuka kuwa mksoaji mkubwa wa utawala wa Rais Ruto.

Baadhi ya viongozi wa ODM kwa upande mwingine wamesikika wakisema chama hicho kitamuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

 

Website |  + posts
Share This Article