Rais William Ruto anasema amejitolea kufanikisha mageuzi katika Muungano wa Afrika (AU), ili kuhakikisha Muungano huo unakuwa taasisi yenye ufanisi zaidi, inayowajibika na kuiitikia maswala mbalimali muhimu.
Akizungumza Ijumaa jioni alipoongoza Mkutano wa Uzinduzi wa Mtandaoni wa Kamati ya Usimamizi ya Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mageuzi ya Taasisi wa AU, alibainisha kuwa mageuzi hayo yataifanya AU ifanikishe kutekeleza matarajio ya Ajenda ya Afrika ya mwaka wa 2063, na kukabiliana na changamoto zinazoendelea kulikabili bara hili.
Alisema mageuzi hayo yanalenga kuimarisha ufanisi wa kitaasisi, kuhakikisha ufadhili endelevu, kurahisisha ufanyaji maamuzi, na kufufua vyombo muhimu vya AU kama vile Bunge la Afrika na Mahakama ya Haki ya Afrika.
Rais Ruto alisema pia wanazingatia kuimarisha utawala, amani, na mifumo ya usalama ya AU ili ibaki kuwa muhimu huku kukiwa na mabadiliko ya mienendo ya kimataifa na migogoro inayoongezeka.
Mkutano huo ulijadili hatua zilizopigwa na kukamilika kwa mageuzi, na kuweka vipaumbele kabla ya Mkutano Maalum huko Luanda, Angola, tarehe 26 Novemba mwaka huu.
