Ruto: Mradi wa barabara wa Last Mile utawaunganisha Wakenya

Tom Mathinji
2 Min Read

Serikali itaongeza umakini wake katika mradi wa ujenzi wa barabara wa Last Mile, ili kuongeza ufikiaji wa rasilimali na huduma.

Rais William Ruto, alisema fedha zaidi zitawekwa katika uboreshaji wa barabara, hatua ambayo pia itachochea biashara mashinani.

Alisema barabara bora zitawahakikishia wakulima, hasa wa mazao mapya, mapato bora.

“Tunapofanya biashara zaidi, inamaanisha fursa nyingi za ajira kwa vijana wetu,” alielezea.

Rais alizungumza hayo jana Alhamisi eneo la Boiman huko Ol Joro Orok alikozindua uwekaji lami katika barabara za Boiman – Kwa Mumbi.

Alisema eneo hilo lenye urefu wa Kilomita 44 ni tegemeo kwa wakulima wa maziwa, mbogamboga na viazi katika kaunti hiyo kwa kuwa linawaunganisha na masoko bora.

Alibainisha kuwa uunganisho wa Last Mile ambao Mamlaka ya Barabara za Vijijini ya Kenya inaendesha utahakikisha kuwa hakuna sehemu yoyote ya nchi iliyoachwa nyuma.

“Kukiwa na barabara bora, Wakenya watapata rasilimali, huduma muhimu na fursa kwa urahisi.”

Rais alisema kazi zingine zinazoendelea katika kaunti hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Kapteni Ndemi – Ndunyu Njeru yenye urefu wa Kilomita 55, ujenzi wa barabara ya kilomita 41 – Gathera, Kilomita 45 Maili Kumi – Shameta, Kilometa 55 Shamata – Uruku, Kilomita 23 Gilgil – Mashine na 28-Kilometa za barabara ya Tumaini -Kabazi.

Zile ambazo zimetengwa kukarabatiwa, aliongezea, ni barabara za Nyahururu Kilometa 14 – Boiman, Kilometa 14 za Maili Nne – Maili Kumi na za Kirasha Kilometa 8 – Sulmac.

Viongozi wliohudhuria hafla hiyo ni Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Waziri Kipchumba Murkomen, Gavana wa Kaunti ya Nyandarua Moses Badilisha, Wabunge na Wawakilishi wa Wadi.

Website |  + posts
Share This Article