Rais Ruto: Malipo ya wakulima wa miwa haitachelewa tena

Tom Mathinji
2 Min Read

Serikali imeanza kulipa Shilingi milioni 300 inayodaiwa na wakulima wa Kiwanda cha Sukari cha Nzoia, Rais William Ruto amesema.

Alisema Shilingi bilioni 1.7 zilizoidhinishwa na wabunge zitasaidia pakubwa mipango ya kufufua sekta ya sukari nchini.

Rais Ruto alisema wakulima wote wa Nzoia watapokea pesa zao katika siku mbili zijazo.

Akizungumza katika uwanja wa Kiwanda cha Sukari cha Nzoia Kaunti ya Bungoma siku ya Alhamisi, Kiongozi wa Nchi alisisitiza kuwa mageuzi yanafanywa ili kuvipa uhai viwanda vya umma vinavyosuasua vya sukari kote nchini.

“Ninataka kuwahakikishia kuwa hali ambayo wakulima wanapeleka miwa yao kiwandani na kutolipwa haitajirudia tena. Hali ambayo wafanyikazi hawajalipwa mishahara haitajirudia tena,” alisema Rais Ruto.

Alisema usimamizi, ambao utachukua mamlaka katika Nzoia lazima, miongoni mwa mengine, uwe tayari kuwalipa wakulima na wafanyikazi kwa wakati kando na kulipa serikali ya kaunti ya Bungoma kati ya Shilingi milioni 300 na Shilingi milioni 500 kila mwaka.

“Nitakutana na viongozi wenu na kukubaliana kuhusu kanuni sahihi kwa sababu kampuni nyingi zilizobinafsishwa zinaweza kuwalipa wakulima na wafanyikazi wao. Hii ina maana kwamba tatizo kuu katika viwanda hivi vya umma ni usimamizi duni na wala si kilimo cha miwa,” alisema Rais Ruto.

Wakati huo huo Kiongozi wa Nchi, aliwahakikishia wakazi kuwa hakuna mipango ya kuuza au kubinafsisha Kiwanda cha Sukari cha Nzoia.

“Ninataka kuwahakikishia kuwa tutakuwa na usimamizi mpya ambao utawalipa wakulima na wafanyakazi madeni na mishahara yao kwa wakati,” akasema Rais Ruto.

Alisema serikali itatenga Shilingi milioni 500 kwa kila moja kwa viwanda vya sukari vya Nzoia, Chemilil, Sony na Muhoroni ili kuongeza uzalishaji.

“Tutaongeza fedha kwa viwanda vinne vya miwa ili kuwawezesha wakulima kuzalisha zaidi ili Kenya ikome kuagiza sukari nchini,” akasema.

TAGGED:
Share This Article