Rais William Ruto anatarajiwa kuanza ziara ya siku tatu katika eneo la Gusii ambalo lina kaunti mbili za Kisii na Nyamira kuanzia leo Jumatatu.
Akiwa katika eneo hilo, Rais anatarajiwa kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara za umbali wa kilomita 64, mpango wa kuunganisha umeme wa Last Mile pamoja na kufutiliwa mbali kwa deni la kiwanda cha majani chai cha Sombogo.
Leo Jumatatu, Rais anatarajiwa kuanzia ziara hiyo katika kaunti ya Nyamira atakapozuru maeneo kama vile shule ya upili ya Kiabonyoru na ile ya Kenyerere kabla ya kuzindua uunganishaji wa umeme katika eneo bunge la Nyaribari chache kaunti ya Kisii.
Rais Ruto atazuru kiwanda cha majani chai cha Sombogo katika eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini kaunti ya Kisii kesho Jumanne kuanzia saa nne asubuhi.
Atazindua pia ujenzi wa kituo cha matibabu ya saratani karibu na shule ya upili ya wavulana ya Kisii na azindue pia barabara inayounganisha eneo la Daraja Mbili na Suneka.
Mnamo siku ya Jumatano ambayo ni siku ya mwisho ya ziara yake katika eneo la Gusii, Rais atazindua ujenzi wa nyumba za gharama nafuu mjini Ogembo eneo bunge la Bomachoge Chache.
Ziara hii ya Rais inajiri baada ya nyingine aliyofanya katika eneo la Mlima Kenya baada ya kuapishwa kwa mawaziri wapya.