Rais Ruto kuzindua miradi ya nyumba Pwani

Rais Ruto yuko katika eneo la Pwani kwa ziara ya kikazi.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto leo Jumatatu anatarajiwa kuzindua miradi kadhaa ya nyumba za bei nafuu ambayo itatoa makazi na fursa za ajira kwa wakazi wengi wa eneo la Pwani.

Miradi hiyo inayotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Maendeleo ya Miji iko katika maeneo ya Mokowe katika kaunti ya Lamu, Tezo katika kaunti ya Kilifi na Voi katika kaunti ya Taita Taveta.

Inatarajiwa kupunguza tatizo la ukosefu wa nyumba za makazi na kutoa nafasi nyingi za ajira.

Katika kaunti ya Taita Taveta, mradi wa nyumba wa Voi Pool utakuwa wa nyumba 458 pamoja na vifaa vingine vya kijamii kama maduka na viwanja vya kuchezea.

Mradi wa Tezo katika kaunti ya Kilifi ndio mkubwa zaidi kwa yote mitatu inayozinduliwa leo, kwani utatoa nyumba elfu moja za makazi katika ardhi ya ekari tano.

Unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 2.5 na unatarajiwa kuchangia shilingi bilioni 1 kwa uchumi wa eneo hilo na ajira ya kudumu kwa watu wapatao 200 katika kipindi cha ujenzi.

Rais William Ruto vile vile amewataka viongozi wa kidini waendelee kuombea nchi ili iendelee kuwa imara na yenye amani.

Akizungumza alipohudhuria ibada ya jioni katika kanisa la Jesus Celebration Centre, huko Bamburi kaunti ya Mombasa jana, Rais Ruto aliwaomba Wakenya waendelee kupendana kulingana na maneno ya wimbo wa taifa.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *