Rais Ruto kutia saini Mswada wa Marekebisho ya IEBC 2024

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto.

Rais William Ruto leo Jumanne atatia saini kuwa sheria Mswada wa Marekebisho ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC wa mwaka 2024. 

Hafla hiyo itafanyika katika jumba la mikutano ya kimataifa la KICC jijini Nairobi.

Mswada huo ulipitishwa na bunge kufuatia mapendekezo yaliyowasilishwa na kamati ya uwiano wa kitaifa kwenye ripoti yake.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed amethibitisha kuwa viongozi wengine wa kisiasa wataungana na Rais wakati wa hafla hiyo.

“Huu ukiwa mswada wa kwanza kushughulikiwa na bunge kufuatia mapendekezo ya ripoti ya kamati ya kitaifa ya mazungumzo NADCO, Rais William Ruto amewaalika viongozi wa kisiasa walio nje na ndani ya bunge kuungana naye katika hafla hiyo ya kihistoria,” alisema Hussein.

Sheria hiyo mpya italainisha utaratibu wa uchaguzi nchini na kutoa fursa ya kuapishwa kwa makamishna wapya wa IEBC.

Viongozi wa upinzani na wale wa kidini wamekuwa wakitoa wito wa kutiwa saini kwa mswada huo ili kutoa fursa ya kuundwa upya kwa tume hiyo.

Katibu wa vyombo vya habari katika Ikulu ya Nairobi Emmanuel Talam alisema kwenye taarifa kwamba kiongozi wa taifa amewaalika viongozi wa vyama vyote vya kisiasa kuhudhuria hafla hiyo ambayo kwa muda mrefu imesubiriwa kwa hamu kuu.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *