Rais William Ruto leo Ijumaa atalihutubia taifa kutoka Ikulu ya Nairobi.
Rais Ruto anatarajiwa kulihutubia taifa majira ya saa kumi jioni.
Hii itakuwa mara ya pili kwa yeye kulihutubia taifa tangu kutangaza kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri siku chache zilizopita.
Ingawa kiini cha haotuba yake haikijawekwa bayana, inatazamiwa kuwa kiongozi wa nchi huenda akawataja mawaziri wapya wakatakaochukua nafasi za wale 21 waliotumuliwa.
Rais Ruto ameahidi kuwataja watu wenye hadhi na haiba watakaomsaidia kutimiza ahadi lukuki alizotoa kwa Wakenya wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Juzi Jumatano, Rais alitangaza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi atakaimu nyadhifa zote za mawaziri waliotumuliwa.
Naibu Rais Rigathi Gachagua na Mudavadi ndio watu pekee ambao walisazwa dhidi ya wembe uliowanyoa mawaziri wote 21 waliofurushwa serikalini.
Kura za maoni zimeonyesha kuwa Wakenya wengi wameunga mkono hatua ya Rais Ruto kuvunjilia mbali Baraza lake la Mawaziri.