Rais Ruto kuhutubia kikao cha pamoja cha bunge Alhamisi

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto atahutubia kikao cha pamoja cha bunge la Taifa la lile la Seneti Alhamisi wiki hii. 

Tangazo hilo limetolewa na Maspika Moses Wetang’ula wa bunge la Taifa na Amason Kingi wa bunge la Seneti leo Jumatatu.

Kifungu 132 (1)(b) na (c) kinamhitaji Rais kuhutubia kikao maalum cha bunge mara moja kwa mwaka.

“Wabunge wote na umma kwa jumla wanataarifiwa kuwa kikao cha pamoja cha bunge kitafanyika katika chemba ya bunge la Kitaifa katika majengo makuu ya bunge, Nairobi, Alhamisi, Novemba 9, 2023 saa nane na nusu mchana,” inasema taarifa kutoka kwa Maspika hao wawili.

Wakati wa kikao hicho, Rais Ruto anatarajiwa kuangazia hatua zinazochukuliwa na utawala wake kuangazia changamoto mbalimbali zinazolikumba taifa ikiwa ni pamoja na gharama ya juu ya maisha.

Serikali imekuwa mstari wa mbele kuwagawia wakulima bei ya mbolea ya bei nafuu na mbegu katika hatua inayolenga kuimarisha uzalishaji wa chakula nchini.

Aidha miradi ya miundombinu inayotekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza chini ya mpango wake wa mabadiliko ya kiuchumi kuanzia chini hadi juu, BETA inatarajiwa kuangaziwa katika hotuba ya Rais.

 

Website |  + posts
Share This Article