Rais Ruto kuanza ziara ya siku tano magharibi mwa nchi

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais Ruto wakati wa ziara yake ya awali magharibi mwa nchi

Rais William Ruto ataanza ziara ya kikazi ya siku tano magharibi mwa nchi kuanzia kesho Jumamosi. 

Rais Ruto atazuru kaunti za Busia, Bungoma, Vihiga, na Kakamega.

Msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed anasema wakati wa ziara hiyo, kiongozi wa nchi atazindua na kukagua miradi ya maendeleo ambayo inawanufaisha Wakenya moja kwa moja, kuendana na ajenda ya serikali ya kutokea chini kwenda juu.

Katika kaunti ya Busia, Rais anatazamiwa kuzindua sehemu ya kuweka samaki baada ya kuvuliwa ya Mulukhoba, kufungua hospitali ya kaunti, na kuzindua maktaba katika Chuo Kikuu cha Alupe.

Katika kaunti ya Bungoma, Rais atazindua ujenzi wa kiwanda cha kuongezea thamani cha Bungoma na kuzuru kampuni ya sukari ya Nzoia miongoni mwa miradi mingine.

Rais pia atazindua hospitali ndogo ya Emuhaya katika kaunti ya Vihiga.

Katika Nkulu Ndogo ya Kakamega, Rais Ruto ataongoza mkutano wa Baraza la Mawaziri na kukutana na wakulima wa eneo hilo.

Ruto analenga kushirikiana kwa karibu na watu na uongozi wa eneo hilo, akisisitiza dhamira yake ya kutekeleza maendeleo magharibi mwa nchi.

Share This Article