Rais Ruto kuanza ziara ya siku nne Mlima Kenya, Jumanne

Dismas Otuke
2 Min Read

Rais William Ruto anatarajiwa kuanza ziara ya siku nne eneo la mlima Kenya kesho hadi Ijumaa hii ambapo atakagua miradi kadhaa ya maendeleo.
Ziara hiyo itakuwa ya kwanza kwa Rais katika eneo hilo, miezi sita tangu amtimue aliyekuwa Naibu Rais wake Rigathi Gachagua anayetoka eneo hilo.

Aidha,Rais atatumia ziara hiyo kujipigia debe na kutafuta uungwaji mkono kutoka eneo hilo katika azma ya kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Rais atazindua miradi kadhaa ya maendeleo eneo hilo na kukagua miradi mingine iliyoanzishwa chini ya mfumo wake wa uchumi wa Bottom Up.

Miongoni mwa miradi atakayozindua Rais ni pamoja na ile ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu,uunganishaji umeme,usambazaji maji na unyunyiziaji mashamba maji miongoni mwa miradi mingine.

Kiongozi wa nchi ameratibiwa kuzuru kaunti tisa za mlima Kenya ikiwa ni;Laikipia, Nyeri, Meru, Kirinyaga, Nyandarua, Murang’a, Embu, Tharaka-Nithi na Kiambu.

Kutanguliza ziara hiyo ya kesho,Rais Ruto atafanya mazungumzo na wa wananchi wa mlima Kenya katika mahojiano ya moja kwa moja kupitia kwa idhaa za lugha ya Kikuyu leo jioni kutoka  Ikulu ndogo ya Sagana.

Idhaa ya Coro FM na idhaa za kimaeneo za KBC zitarusha mubashara mahojiano hayo.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake kesho Rais atazuru maeneo bunge ya Rumuruti, Laikipia West , Nanyuki, Laikipia East na hatimaye Naromuro katika eneo bunge la Kieni .

Website |  + posts
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *