Rais William Ruto amesema Kenya na Zambia zitaimarisha uhusiano wao ili kupanua biashara na utalii kati ya raia wa nchi hizo mbili.
Akizungumza aliposhauriana na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema pembezoni mwa mkutano wa COMESA unaoendelea jijini Bunjumbura nchini Burundi, kiongozi wa taifa alisema Kenya na Zambia zinafurahia urafiki wa muda mrefu, tangu mataifa hayo kupata uhuru miaka 60 iliyopita.
“Nchi hizi mbili pamoja na raia wake, zinafurahia uhusiano kupitia biashara na ushirikiani wa serikali hizo mbili,alisema Rais Ruto kupitia ukurasa wa X.
Rais Ruto alidokeza kuwa Kenya imejitolea kuimarisha ushirikiano wake na Zambia kupitia wafanyabiashara wa mataifa hayo.
Wakati huo huo Rais Ruto alishauriana na mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika Moussa Faki na katibu mtendaji wa Tume ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika.
Rais William Ruto yuko nchini Burundi kuhudhuria mkutano wa 23 wa COMESA, ambao umewaleta pamoja zaidi ya wawakilishi 400 kutoka sekta ya kibinafsi, wafanyabiashara wadogo, wabuni sera na mashirika ya kijamii.