Rais William Ruto ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasheria maarufu wa masuala ya familia, wanawake na watoto Judy Thongori.
Thongori alifariki jana Jumanne jioni wakati akitibiwa nchini India.
“Tunaungana na familia, marafiki, na tasnia ya uanasheria katika kuomboleza kifo cha Mwansheria Mwandamizi Judy Thongori, mwanasheria wa kipekee na mtetezi wa haki,” amesema Rais Ruto.
“Kujitolea kwake kwa masuala ya sheria ya familia na haki za kibinadamu kuligusa maisha ya wengi na kuacha athari ya kudumu katika jamii yetu. Tutakosa sana na kukumbuka ukarimu, hekima na huduma ya Judy.”
Mwingine aliyemwomboleza Thongori ni Jaji Mkuu Martha Koome ambaye amemtaja mwenda zake kuwa miongoni mwa wanasheria maarufu zaidi humu nchini.
“Bi. Thongori alikuwa mtambaazi katika tasnia ya sheria na mtetezi wa haki mwenye shauku, hasa katika masuala yanayoathiri familia, wanawake na watoto,” alisema Koome kwenye taarifa.
Jaji Mkuu alielezea walivyofanya kazi pamoja Thongori katika Chama cha Wanawake Wanasheria nchni, FIDA-Kenya, miaka ya mwishoni mwa 1990 na mapema 2000 akisema ni wakati huo ambapo marehemu alidhihirisha kuwa mweledi na mchapa kazi aliyejitolea.
Thongori alifahamika sana kutokana uweledi wake katika masuala ya sheria hususan ile iliyohusiana na masuala ya familia, wanawake na watoto.
Marehemu alikuwa mwasisi wa kampuni ya wanasheria ya Judy Thongori aliyoainzisha yamkini miaka 21 iliyopita.
Aliteuliwa kuwa mwanasheria mwandamizi miaka minne iliyopita kutokana na kazi yake maridhawa katika tasnia ya uanasheria.