Rais William Ruto amezomea mawaziri, makatibu wa wizara na wasimamizi wa kampuni za serikali waliochelewa kufika Ikulu ya Nairobi kwa ajili ya hafla ya kutia saini mikataba ya utendakazi.
Kiongozi wa nchi amewataka wote waliochelewa waeleze kwa maandishi ni kwa nini walichelewa na wasitaje msongamano wa magari barabarani.
Alisema wafanyakazi wote wa umma wanafaa kuzingatia kazi zao na hilo linajumuisha kufika kwenye mikutano kwa wakati.
Mawaziri, makatibu wa wizara na wakuu wa kampuni za serikali waliochelewa walifungiwa nje ya Ikulu.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Kirinyaga ni mmoja wa waliochelewa na hotuba yake ilisomwa na Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka.
Mikataba ya utendakazi ni chombo cha usimamizi kilichoanzishwa na serikali ili kusaidia kuendesha sekta ya utendakazi wa umma.
Iliratibishwa na amri nambari 1 ya Januari 6, 2023, na inasimamiwa na afisi ya waziri aliye na mamlaka makuu.
Hii sio mara ya kwanza Rais Ruto anachukua hatua dhidi ya wanaochelewa. Ijumaa, Januari 6, 2023, makatibu wa wizara watatu waliochelewa kufika kwenye mkutano wa Baraza la Mawaziri huko Mount Kenya Safari Club walizomewa.