Rais William Ruto leo amezindua rasmi tawi la Teso la Taasisi ya Mafunzo ya Kimatibabu Nchini KMTC, anapoendeleza ziara ya kikazi magharibi mwa nchi.
Kiongozi wa nchi alizindua pia ujenzi wa mabweni katika tawi hilo la Teso la KMTC, chini ya mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini.
Alisema kwamba vijana hawafai kuchukuliwa tu kama mashine za kupiga kura na kusahaulika punde baada ya uchaguzi, akisema wao ni nguzo muhimu kwa uthabiti wa kijamii na kiuchumi.
Kutokana na hilo alisema serikali imeamua kuwekeza katika elimu, ustawishaji wa ujuzi na biashara ndogo na za kadri ili vijana waweze kuafikia uwezo wao kamili.
Rais Ruto aliweka jiwe la msingi wa ujenzi wa mabweni hayo ya jumla ya vitanda 340 kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.5.
Katika hotuba yake, kiongozi wa nchi alitaja wajibu muhimu unatekelezwa na wanafunzi wa kozi za kimatibabu katika kuafikia mpango wa huduma bora za afya kwa wote na haja iliyopo ya kuwapa mazingira bora ya masomo.
Rais alikuwa ameandamana na uongozi wa KMTC, Gavana wa Busia Paul Otuoma, Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula, Waziri Wycliffe Oparanya na wengine wengi.