Rais William Ruto jana alizindua hospitali maalum ya kushughulikia majeruhi ya Nyabondo katika eneo bunge la Nyakach kaunti ya Kisumu ambayo itaimarisha huduma za afya katika eneo hilo.
Hospitali hiyo ina vitanda 150 na ina vifaa vya kisasa vya matibabu kama vyumba vya upasuaji na vya kuhudumia wagonjwa mahututi ambavyo vimeundwa kwa njia ya kipekee ya kushghulikia wanaojerihiwa kwenye ajali.
Kituo hicho cha afya kitahudumia watu wapatao milioni 5 wa eneo zima la Nyanza.
Huku akishukuru umoja wa Ulaya EU kwa kusaidia kuweka vifaa hospitalini humo, Rais Ruto alisema kwamba shilingi milioni 500 zilizotolewa na umoja huo zimesaidia sana kujenga kituo hicho.
Kiongozi wa taifa alisema hospitali hiyo itakuwa muhimu kwa wanaohitaji huduma za dharura kwa wanaozihitaji hasa majeruhi wa ajali.
Mamlaka inayosimamia barabara kuu nchini KeNHA ndiyo ilijenga kituo hicho kama sehemu ya ukarabati wa barabara ya kutoka Isebania kuelekea Kisii na Ahero.
Kando na kuimarisha huduma za afya katika kaunti za Kisumu, Siaya, Homa Bay, Migori, Kisii na Nyamira, hospitali hiyo pia itapunguza msongamano katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Jaramogi Oginga Odinga, ile ya Kisii na ya Moi jijini Eldoret.
Wagonjwa wanaohitaji huduma za kiwango cha juu hupelekwa kwenye hospitali hizo.
Rais alikuwa ameandamana na viongozi kadhaa akiwemo Naibu Rais Rigathi Gachagua, waziri wa Afya Debra Barasa, Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o na wengine.