Huduma ya taifa ya polisi NPS imekanusha madai kwamba maafisa wa polisi waliiba vipakatalishi kutoka madukani jijini Nairobi wakati wa maandamano ya kulalamikia mauaji ya mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang.
Katika taarifa, NPS imeelezea kwamba inafahamu kuhusu video inayosambaa mitandaoni inayoonyesha afisa mmoja wa polisi akiwa amebeba vipakatalishi hivyo.
“Huduma ya taifa ya polisi ingependa kufafanua kwamba kufuatia maandamano ya jana jijini Nairobi, duka nyingi zilivamiwa na bidhaa mbali mbali kuibwa” ilisema taarifa hiyo.
Mkurugenzi wa mawasiliano katika NPS Muchiri Nyaga aliendelea kusema kwamba polisi hao walikamata mshukiwa mmoja na kumpokonya vifaa hivyo vya kielektroniki, ambavyo vimehifadhiwa katika kituo cha polisi cha Central Nairobi kama ithibati.
“Kwa hivyo tunaomba yeyote ambaye duka lake lilivunjwa na vipakatalishi kuibwa, afike katika kituo hicho cha polisi kuvitambua,” ilihimiza taarifa hiyo.
Huduma hiyo ya taifa ya polisi imesema inaendeleza uchunguzi kwa lengo la kukamata waliohusika ba visa vya uhalifu wakati wa maandamano ya jana, ili wachukuliwe hatua za kisheria.