Rais William Ruto ametoa changamoto kwa wakosoaji wa serikali kuhakikisha wanakuwa wakweli katika ukosoaji wao.
Akizungumza alipoongoza mahafali ya kwanza ya chuo kikuu cha Tangaza jijini Nairobi, Rais alisema kwamba serikali inashirikiana na viongozi wote wakiwemo wa dini ili kuhakikisha ufanisi wa taifa hili.
Usemi wake unajiri siku moja tu baada ya serikali kukosolewa na maaskofu wa kanisa katoliki kuhusiana na kile walichokitaja kuwa ahadi ambazo hazijatimizwa, ukiukaji wa haki za binadamu na kukosa kuunda tume ya uchaguzi na mipaka IEBC.
Maaskofu hao walionya kwamba migogoro iliyopo serikalini imeongeza migawanyiko kati ya wakenya na kusababisha kutoaminiana kati ya wananchi na serikali.
Walifanya kikao na wanahabari katika makazi ya wachungaji ya parokia ya Queen of Apostles huko Ruaraka, ambapo walionekana kupinga pendekezo la kuongeza muda wa kuhudumu wa viongozi waliochaguliwa.
Walikosoa pia mabadiliko ya bima ya kitaifa ya afya kutoka NHIF hadi SHIF.
Lakini katika usemi wake wa leo, Rais Ruto alisema pia kwamba serikali imejitolea kuimarisha ujumuishaji na elimu bora ya vyuo vikuu nchini.
Alisisitiza kuhusu mageuzi yanayolenga kuhakikisha ufadhili endelevu, unaopatikana kwa wote na mifumo imara ya utafiti na uvumbuzi.