Rais Ruto awapandisha vyeo wakuu kadhaa wa jeshi

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amefanya mabadiliko kadhaa katika uongozi wa jeshi ambapo wengine wamepandishwa vyeo huku wengine wakiteuliwa.

Uamuzi huu unafuatia ushauri aliopokea Rais kutoka kwa baraza la ulinzi nchini ambalo lilikutana chini ya uenyekiti wa kaimu waziri wa ulinzi nchini Musalia Mudavadi.

Baada ya kuvunja baraza la mawaziri, Rais Ruto alimteua Mudavadi kuhudumu kama kaimu waziri katika wizara zote nchini hadi mawaziri watakapoteuliwa tena.

Katika mabadiliko ya leo, Meja Jenerali Stephen James Mutuku ameteuliwa kuwa naibu kamanda wa taasisi ya kitaifa ya mafunzo ya ulinzi nchini.

Makanali kadhaa pia wamepandishwa vyeo na kuwa mabrigedia kabla ya kuteuliwa kusimamia vitengo mbali mbali ambapo Edward Morris Ondabu Nyamao ameteuliwa kuwa mkuu wa masuala ya fidia na maslahi katika jeshi.

Collins Otieno Mitoko ameteuliwa kuwa mkuu wa wafanyakazi katika makao makuu ya jeshi la taifa huku Paul Kiplimo Koech akiteuliwa kuwa mkuu wa mafunzo.

Clement Kimaiga Nyakundi ameteuliwa kuhudumu kama naibu meneja mkuu wa kampuni ya nyama nchini KMC na Victor Ndegwa Mburu naye amejukumiwa kuwa kamanda wa kitengo cha wahandisi wa jeshi la Kenya.

Eric Nzioki Kitusya atasimamia masuala ya vifaa, Salaash Kantai ndiye kamanda wa kikosi cha majasusi wa jeshi, Edward Willy Banda ameteuliwa kamanda wa kikosi nambari 8 na Jackson Lesaiyo Lemakara sasa ndiye kamanda wa kituo cha Embakasi Garrison katika baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa katika jeshi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *