Katika jumbe mbili tofauti kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Rais William Ruto ametuma salamu za rambirambi kwa Gavana na Naibu Gavana wa kaunti ya Meru ambao wamefiwa na wapendwa wao.
Mapema asubuhi, kiongozi wa nchi alituma risala za rambirambi kwa Naibu Gavana wa kaunti ya Meru Isaac M’Ethingia ambaye amefiwa na mamake mzazi.
“Pole zetu kwa Naibu Gavana wa kaunti ya Meru Isaac M’Ethingia kwa kumpoteza mama mzazi, Joyce,” aliandika kiongozi wa nchi huku akimtaja marehemu kuwa mama aliyewajibika, aliyemwamini Mungu na mwenye maendeleo aliyejitolea kuhudumia jamii.
“Mungu aifariji familia na watu wa Meru wakati huu wa huzuni. Lala salama.”
Baadaye alasiri, kiongozi wa nchi alichapisha ujumbe mwingine wa pole kwa Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza aliyefiwa na kakake kwa jina Eric Kimathi maarufu kama ‘Steroo’.
“Tunasherehekea maisha ya jamaa mfanyabiashara aliyekuwa na mawazo mazuri yaliyobadilisha maisha ya wengi,” alisema Rais Ruto akiongeza kwamba ‘Steroo’ alikuwa mkarimu, mwenye bidii na mwenye maendeleo.
Gavana Mwangaza amemshukuru kiongozi wa nchi kwa kuwazia familia zao, na jamii nzima ya kaunti ya Meru wakati huu wa majonzi.
Alimtaja kuwa Rais bora kwa kuwakumbuka.