Rais William Ruto Ijumaa jioni aliondoka humu nchini kuelekea Addis Ababa nchini Ethiopia, kwa mkutano wa viongozi wa mataifa mbalimbali na serikali barani Afrika .
Kupitia mtandao wake wa kijamii , hatibu wa Rais Hussein Mohamed alisema rais anatarajiwa kuzungumzia ukosefu wa usawa katika sekta ya elimu barani Afrika, ambao umesababisha watoto milioni 98 kukosa elimu barani humu.
Rais Ruto pia anatarajiwa kuwasilisha ripoti kuhusu hatua zilizopigwa na bara hili katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa zikiwa ni pamoja na mkataba wa Nairobi, ulioafikiwa kwenye mkutano wa kwanza kuhusu hali ya hewa uliofanyika jijini Nairobi mwezi Septemba mwaka uliopita.
Rais pia atashiriki kongomano ndogo la Afrika Mashariki, litakaloangazia hali ya amani katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, miongoni mwa maswala mengine.
Rais pia atafanya mazungumzo na marais wengine, viongozi wa mashirika ya kimataifa pamoja na viongozi wa kibiashara.