Rais William Ruto ametoa onyo kali kwa kampuni zinazodaiwa kuhodhi mafuta kwa lengo la kuyauza punde bei ya bidhaa hiyo itakapopanda.
Amesema utawala wake kamwe hautakubali kuwepo uhaba bandia wa mafuta nchini kwa sababu ya baadhi ya kampuni kujihusisha katika uovu huo.
Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatano, Ruto amesema serikali yake tayari imeanzisha mazungumzo na wadau wa humu nchini na wa kikanda kwa lengo la kutafuta namna ya kushughulikia suala la mafuta ambalo kiini chake ni mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.
“Pia tumezielezea wazi kampuni za mafuta na wale ambao wana uwezo wa kuhifadhi mafuta kwamba serikali ya Kenya haitakubali kusababishwa kwa uhaba bandia wa mafuta unaokusudiwa kuwanufaisha watu fulani,” alisema Ruto wakati wa kutiwa saini kwa mikataba ya pande mbili kati ya Kenya Msumbiji.
“Tutakuwa makini zaidi na wadau wote kuhakikisha kila mshiriki anazingatia masharti ya utoaji leseni ili tusizidishe au kuongeza athari hasi lakini badala yake kuepusha na kupunguza athari hizo.”
Rais Ruto aliyasema hayo wakati ambapo baadhi ya kampuni za mafuta zimeripoti ongezeko la mahitaji ya mafuta nchini, hali ambayo zinasema imesababisha uhaba wa muda.
Kwenye taarifa, kampuni ya Vifo Energy Kenya inayosambaza na kuuza bidhaa za Shell ilisema mahitaji ya bidhaa zake yameongezeka na hivyo kusababisha uhaba wa muda wa bidhaa hizo.
“Tumeshuhudia ongezeko la mahitaji hivi karibuni, ambayo yamesababisha uhaba wa muda wa bidhaa zetu katika baadhi ya vituo,” ilisema Vifo Energy Kenya.
“Timu zetu zinafuatilia hali hiyo kwa karibu na kufanya kazi kwa udi na uvumba kujaza upya mafuta katika vituo vilivyoathiriwa haraka iwezekanavyo.”
Kwa upande wake, kampuni ya ndege ya Skyward Airlines ilitangaza kuwa itaongeza nauli kuanzia Aprili 1 kutokana ongezeko la bei za mafuta.
Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati umevuruga usambazaji wa mafuta duniani, hali ambayo imesababisha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.
Nchi nyingi pia zimeazimia kutumia akiba yake ya mafuta kukabiliana na uhaba unaotarajiwa kushuhudiwa duniani kote.
Mgogoro huo ulianza baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran ambayo imeapa kuendelea kujibu mashambulizi hayo.
Iran imekanusha madai ya Rais Donald Trump kwamba inashiriki mazungumzo yanayolenga kutatua mgogoro huo.