Rais William Ruto leo Ijumaa ametia saini kuwa sheria Mswada wa Ugavi wa Mapato kwa Serikali za Kaunti 2024.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema hatua hiyo itahakikisha serikali za kaunti zinatekeleza majukumu yake kwa raia iapasavyo.
Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Waziri wa Fedha John Mbadi na Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi ni miongoni mwa viongozi walioshuhudia utiaji saini mswada huo.
Mswada wa Ugavi wa Mapato kwa Serikali za Kaunti 2024 unagawa kwa usawa shilingi bilioni 387.4 zilizotengewa serikali 47 za kaunti kwa mujibu wa utaratibu wa ugavi wa mapato uliowekwa na kifungu 217 cha katiba.
Fedha hizo ni sawa na asilimia 24.7 ya ukaguzi wa fedha zilizopokokelewa kama zilivyoidhinishwa na Bunge la Kitaifa.
Kiasi hicho cha fedha kinazidi kiwango cha asilimia 15 kilichowekwa na katiba,
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo Magavana wamekuwa waikiilaumu serikali kuu kwa kuchelewa kutoa mgao wa fedha zilizotengewa serikali za kaunti.
Kulingana nao, hatua hiyo imeathiri kwa kiwango kikubwa utendakazi wa serikali zao kwa raia na kuchelewesha utekelezaji wa miradi muhimu.
Aidha, Rais Ruto ameutia saini mswada huo kuwa sheria wakati ambapo Magavana wamekanusha vikali taarifa zilizochapishwa na Mdhibiti wa Bajeti kuashiria kuwa kaunti kumi hazikutumia hela zilizotengewa katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Magavana amesema kuwa kaunti hazingetumia hela hizo kwani zilikuwa hazijatolewa na hazina kuu.
Mdhibiti wa Bajeti Dkt. Margaret Nyakang’o kwenye ripoti yake alisema kuwa kaunti 10 hazikutumia hata senti moja walizotengewa katika miezi ya Julai, Agosti na Septemba.
Abdullahi ameitaja ripoti hiyo kuwa yenye nia mbovu na iliyolenga kuchafua sifa za Magavana, wakati ambapo serikali kuu ilichelewesha utoaji wa pesa hizo.
Kaunti zilizomulikwa katika ripoti hiyo ni:- Nairobi, Baringo, Elgeyo Marakwet, Kajiado, Kisii,Lamu, Uasin Gishu, Nyandarua, Tana River na West Pokot.