Rais Ruto ateua mawaziri wapya huku akifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri

Hanna Wendot Cheptumo ameteuliwa kuwa waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na urithi na Goeffrey K.Ruku akateuliwa waziri wa utumishi wa umma, ustawishaji wa nguvu kazi na mipango maalum.

Marion Bosire
2 Min Read
Geoffrey Ruku na Hanna Wendot Cheptumo

Katika taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumatano Machi 26, 2025, iliyotiwa saini na mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei, Rais William Ruto ametangaza uteuzi wa mawaziri wawili wapya.

Hanna Wendot Cheptumo ameteuliwa kuwa Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi. Wadhifa huu umesalia wazi tangu Rais William Ruto alipofanya mabadiliko ya kwanza katika Baraza lake la Mawaziri na kumwondoa aliyekuwa Waziri Aisha Katana Jumwa.

Kiongozi wa taifa alipofanya uteuzi wa mawaziri wapya, Bi. Stella Soi Lang’at aliyekuwa ameteuliwa kuhudumu kwa wadhifa huo alikataliwa na bunge baada ya usaili.

Mbunge wa Mbeere Kaskazini Goeffrey K.Ruku ameteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Utumishi wa Umma, Ustawishaji wa Nguvu Kazi na Mipango Maalum ambapo atachukua mahali pa Justin Muturi ambaye amepigwa kalamu.

Wateuliwa hao wapya wanatarajiwa kuidhinishwa rasmi kuhudumu katika nyadhifa hizo baada ya usaili katika bunge la kitaifa.

Katika mabadiliko mengine, Rais William Ruto amemhamishia Waziri wa Afya Deborah Barasa katika Wizara ya Mazingira huku Waziri wa Mazingira Aden Duale akipelekwa kuhudumu katika Wizara ya Afya.

Kiongozi wa nchi anatumai kustawisha hata zaidi Baraza lake la Mawaziri kufuatia uteuzi huu pamoja na mabadiliko ili kuafikia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika taifa la Kenya.

“Wawili hawa walioteuliwa wanatarajiwa kuleta kwa baraza la mawaziri ujuzi na uzoefu wao kutokana na taaluma zao pamoja na hekima waliyojikusanyia katika maisha yao,” ilisema taarifa ya Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.

Rais amewapongeza pia kwa uteuzi wao huku akiwatakia mema katika mchakato mzima wa kuidhinishwa na bunge ambao ni timizo la mahitaji ya kisheria ya katiba ya Kenya.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *