Rais Ruto ateua makatibu wapya wa idara za serikali

Rais amesema amewasilisha majina ya wateuliwa hao kwa bunge kwa ajili ya kusailiwa kabla ya kuidhinishwa.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais William Ruto.

Katika mabadiliko ya hivi punde zaidi serikalini, Rais William Ruto ameteua makatibu kadhaa wa idara za serikali.

Jane Kare Imbunya ameteuliwa kuhudumu katika idara ya utumishi wa umma na maendeleo ya nguvu kazi, Regina Akoth Ombam idara ya biashara na Cyrell Wagunda Odede idara ya uwekezaji wa umma na usimamizi wa mali ya umma.

Caroline Wanjiru Karugu ambaye aliwahi kuwa naibu Gavana wa kaunti ya Nyeri ameteuliwa kuhudumu katika idara ya masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, maeneo kame na maendeleo ya kimaeneo.

Katibu mkuu wa zamani wa chama cha madaktari, wanafamasia na wataalamu wa meno KMPDU Ouma Oluga ameteuliwa kuwa katibu katika idara ya huduma za Afya ambapo anachukua mahala pa Harry Kimutai.

Idara ya Uratibu wa shughuli za serikali ya kitaifa itakuwa chini ya Ahmed Abdisalan Ibrahim, idara ya haki, haki za binadamu na masuala ya katiba itasimamiwa na Judith Naiyai Pareno, huku Bonface Makokha akiteuliwa katibu wa idara ya mipango ya kiuchumi.

Profesa Abdulrazak Shaukat ameteuliwa katibu wa idara ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi, Stephen Isaboke katibu wa idara ya utangazaji na mawasiliano, Michael Lenasalon idara ya ugatuzi na Fikirini Katoi Kahindi idara ya masuala ya vijana.

Wengine walioteuliwa ni Carren Ageng’o Achieng idara ya maslahi ya watoto na Aden Abdi Millah idara ya uchukuzi wa majini na shughuli za majini.

Katika mawasiliano yake leo, Rais amesema amewasilisha majina ya wateuliwa hao kwa bunge kwa ajili ya kusailiwa kabla ya kuidhinishwa.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *