Rais William Ruto ametetea ujenzi wa kituo cha kuwatenga wagonjwa wa Ebola raia wa Marekni katika kaunti ya Laikipia, akisema kituo hicho kinalenga kuimarisha afya ya umma na uwezo wa nchi hii wa kukabiliana na changamoto ibuka.
Ruto amefananisha ujenzi wa kituo hicho na hatua zilizochukuliwa wakati wa janga la Covid-19, ambapo kituo cha kuwatenga walioambukizwa kilijengwa katika hospitali ya Nairobi kudhitibi ugonjwa huo.
Matamshi yake yanajiri siku chache baada ya Mahakama Kuu kuzuia kwa muda ujenzi wa kituo hicho na kuwasili kwa watu walioambukizwa Ebola hapa nchini, hadi kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Akizungumza na wanahabari katika Ikulu ndogo ya Wajir, Ruto aliwasihi viongozi na wadau wengine kutoingiza siasa kwenye afya ya umma, huku akielezea kujitolea kwa serikali kulinda afya ya Wakenya wote.
“Kituo cha karantini kinachojengwa katika kambi ya jeshi la wanaanga la Laikipia kwa ushirikiano na serikali ya Marekani, kinalenga kulinda afya ya umma na kuimarisha uwezo wetu wa kukabiliana na dharura za afya,” alisema Rais Ruto.
Alisema utawala wake umechukua hatua zote zinazohitajika kuzuia, kugundua na kudhibiti visa vyovyote, huku ukiimarisha uwezo wa kukabiliana na changamoto za afya ya umma kwa msaada wa washirika wa kimataifa.
“Ushirikiano wa Kenya na Marekani umedumu kwa miongo kadhaa na umetekeleza jukumu muhimu katika kukabiliana na changamoto za kiafya ikiwa ni pamoja na HIV/AIDs, COVID-19, na Ebola”, alidokeza Rais Ruto.
Jana Jumatatu, wakazi wa Nanyuki waliandamana kupinga ujenzi wa kituo hicho, wakiapa kuendelea na maandamano hayo hadi ujenzi huo utakaposimamishwa.
Kenya haijanakili kisa chochote cha Ebola, lakini taifa jirani la Uganda limenakili visa 9, hatua ambayo imesababisha nchi hiyo kufunga mpaka wake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.