Rais William Ruto, amezungumza kwa njia ya simu na waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, ambapo wamejadiliana maswala kadhaa yanayohusu nchi hizo mbili.
Kupitia Ukurasa wa X, kiongozi wa taifa alisema mazungumzo hayo ya Jumanne jioni, yaliangazia biashara, usalama na amani katika kanda hii.
Rais alisema walijadili haja ya Marekani kuunga mkono soko huru la AGOA ambalo ni mkakati muhimu kati ya Marekani na Afrika.
Alisema waliangazia hali ilivyo nchini Haiti, huku waziri Rubio akithibitisha Marekani itaendelea kuunga mkono juhudi za kuleta amani nchini humo zinazoongozwa na Kenya.
Kuhusu hali ya usalama katika kanda hii, Waziri Rubio alishukuru Kenya kwa jukumu muhimu inalotekeleza katika kutafuta amani na kutatua mizozo.
“Nilimfahamisha kuhusu mkutano wa pamoja kati ya Marais wa EAC na SADC kuhusu juhudi za kuleta amani nchini DRC, ulioandaliwa Jumatatu,” alisema Rais Ruto.
Kuhusu mzozo unaoshuhudiwa Sudan Kusini, Rais Ruto alisema alimfahamisha waziri Rubio kuhusu haja ya serikali na upinzani kujadiliana kusitisha vita na kuhakikisha amani inadumu.
Kiongozi wa taifa alisema alimjulisha Rubio kuhusu shughuli za kigaidi nchini Somalia na haja iliyopo kwa Kenya na Marekani kushirikiana kukabiliana na tisho hilo kwa manufaa ya nchi hizo mbili na jamii ya kimataifa kwa jumla.
Mazungumzo hayo ni ishara kwamba uongozi wa ushirikiano katika ya Kenya na Marekani katika kushughulikia changamoto zinazozikabili na kuimarisha manufaa ya pamoja.