Rais William Ruto amewataka wazazi kutunza wanao vyema kama sehemu ya juhudi za kushughulikia maovu katika jamii.
Kiongozi wa nchi aliyasema hayo jana katika kaunti ya Mombasa alikohudhuria harusi. Alisema wanaotekeleza uhalifu kote nchini, ni watoto waliopotoka kimaadili.
Aliwataka wazazi hao kuwafunza wanao neno la Mungu la kuwapa ushauri unaofaa dhidi ya matendo mabaya.
Rais Ruto alisema inasikitisha kuona kwamba wazazi wengi wanaachia serikali majukumu yao ya malezi ambayo serikali haiwezi kutekeleza.
Aliwataka wawaelekeze wanao kwa njia inayofaa.
Ushauri wa rais unajiri wakati ambapo kuna ripoti za kuibuka tena kwa magenge ya wahalifu katika kaunti ya Mombasa na maeneo ya karibu.
Wakazi wa maeneo kama Mvita, Kisauni, Jomvu, Changamwe, Nyali na Likoni wamelalamikia uvamizi unaotekelezwa na magenge hayo huku ripoti zikiashiria kwamba yanahusisha vijana wadogo wa hadi umri wa miaka kumi pekee.