Rais William Ruto amesema kwamba serikali imejitolea kuhakikisha upatikanaji wa maji safi ya kunywakwa wakenya zaidi, hasa wakazi wa kaunti ya Nairobi.
Akizungumza katika kanisa katoliki la Soweto huko Kayole kaunti ya Nairobi alikohudhuria ibada, kiongozi wa taifa alisema kwamba hivi karibuni atazindua handaki la kaskazini la kuhifadhi maji.
Handaki hilo amelitaja kuwa mradi muhimu katika kuboresha usambazaji wa maji katika kaunti ya Nairobi na maeneo jirani.
Rais alisema pia kwamba serikali yake iko macho kuimarisha miundombinu ya elimu Nairobi ambapo ameahidi sshilingi bilioni moja za kugharamia ujenzi wa madarasa.
Chini ya mradi huo, kila eneo bunge katika kaunti ya Nairobi litapata shilingi milioni 58 za kujenga madarasa 30 zaidi.
Kiongozi wa taifa alielekeza kwamba matumizi ya uwanja wa Jacaranda yabadilishwe na eneo hilo litumike kujenga shule ya msingi na ya sekondari.
Kuhusu bima mpya ya afya, Rais alisema kwamba ana imani kwamba itafaulu na kila mkenya aweze kupokea matibabu ipasavyo.
Kwa mara nyingine Rais alitoa hakikisho kwa maaskofu wa kanisa katoliki kwamba atashirikiana na wadau wote kuhakikisha kwamba bima mpya ya afya inafanikishwa.
Alisema serikali imelipa shilingi bilioni 5 na wiki hii itaongeza bilioni 2 ili kuhakikisha vituo vyote vya afya vya umma vimefadhiliwa ili kufanikisha mpango wa afya kwa wote.