Rais William Ruto amepongeza uhusiano unaoimarika kati ya Kenya na Sudan Kusini, huku akiwa mwenyeji wa Rais wa taifa hilo anayezuru Kenya Salva Kiir katika Ikulu ya Nairobi.
“Tulielezea kuridhishwa kwetu na uhusiano thabiti kat ya mataifa hayo mawili na kuazimia kuendelea kubuni fursa zaidi za kibiashara na uwekezaji kwa raia wetu,” alisema Rais Ruto kwenye ukurasa wa X.
Aidha, Ruto alimpongeza Rais Kiir kwa ushiriki wa Sudan Kusini katika uzinduzi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote katika kaunti ya Lamu juma lililopita.
Wakati huo huo alipongeza taifa hilo changa zaidi barani Afrika linapojiandaa kuandaa Uchaguzi Mkuu mwezi Disemba 2026, ambao ni wa kwanza tangu nchi hiyo ilipopata uhuru Julai 9, 2011.
“Kenya iko tayari kuiunga mkono Sudan Kusini, huku ikitoa wito wa mazungumzo na makubaliano kati ya pande zote husika,” aliongeza Rais Ruto.