Rais Ruto apongeza idhini ya UNSC ya kupelekwa kwa polisi Haiti

Tom Mathinji
2 Min Read

Rais William Ruto amepongeza hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC ya kuidhinisha kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa cha maafisa wa usalama kukabiliana na utovu wa usalama nchini Haiti.

Kulingana na Rais Ruto, Kikosi hicho kitapiga jeki juhudi za huduma ya taifa ya polisi nchini Haiti kukabiliana na makundi ya wahalifu.

“Kikosi hicho ni muhimu katika kuhakikisha mazingira bora kwa Haiti, kufanikisha maendeleo na kurejesha uongozi. Ni muhimu kwa kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa, UN nchini Haiti kuwa na rasilimali zinazohitajika,” alisema Rais Ruto.

Rais alisema kutumwa kwa kikosi hicho kutasaidia pakubwa katika kulinda miundombinu muhimu nchini Haiti, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege, bandari na mifumo mingine ya usafiri.

Rais alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, mashirika ya kimataifa na taasisi zingine kusaidia kuokoa mazingira yanayozorota nchini Haiti, hali ambayo inapaswa kushughulikiwa kwa dharura.

“Hatua hii ni ya kibinadamu ambayo inaambatana na sera za UN kuhakikisha kuna matumaini kwa watu wa Haiti,” aliongeza Rais Ruto.

Kikosi hicho kipya kitafanya operesheni za pamoja za usalama na kitakuwa na mamlaka ya kukamata watu kwa ushirikiano na polisi wa Haiti, kulingana na azimio hilo.

Kwa miongo kadhaa, Haiti imekumbwa na ghasia zinazofanywa na magenge ya wahalifu lakini wimbi la ukatili liliongezeka baada ya mauaji ya aliyekuwa Rais nchi hiyo Jovenel Moïse Julai, 2021.

Share This Article