Rais Ruto amtunuku Raila tuzo ya Rais ya kiwango cha juu zaidi

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto hii leo amemtambua kwa njia ya pekee na kumuenzi marehemu waziri mkuu wa zamani Raila Amolo odinga katika sherehe za mwaka huu za siku kuu ya Mashujaa huko Kitui.

Kiongozi wa nchi alitangaza utambuzi huo ambao ni tuzo inayofahamika kama “Chief of the Order of the Golden Heart” hatua ambayo tayari imeratibishwa kupitia arifa ya gazeti rasmi la serikali.

Katika toleo hilo nambari 15198 la leo Oktoba 20, 2025, Rais Ruto alimtaja Raila kuwa mmoja wa wasanifu wakuu wa mpangilio wa kisasa wa dmokrasia nchini.

“Ikitizamiwa kwamba Raila Amolo Odinga alijitolea kikamilifu kutafuta haki, uhuru na usawa wa kimaendeleo nchini Kenya na maendeleo ya kila mwananchi” alisema Rais kwenye arifa hiyo akiorodhesha sababu za kumtunuku mwendazake heshima hiyo.

Rais alisema Raila alihudumia taifa hili katika nyanja mbali mbali kama vile uhadhiri katika chuo kikuu cha Nairobi, mbunge, waziri, kiongozi wa upinzani na waziri mkuu wa pili wa Kenya.

Ruto alitaja pia jumbe za rambirambi na maombolezi kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu kufuatia kifo cha Raila kuwa ishara ya ushawishi aliokuwa nao kote nchini na hata nje.

Rais William Samoei Ruto alitoa heshima hiyo kutokana na ushawishi aliopatiwa na kifungu nambari 132 sehemu ya 4 (c) cha katiba ya Kenya kumtambua Raila hata baada ya kifo chake.

Kiongozi wa nchi ameendelea kutoa heshima kwa mwendazake kwa kuahirisha shughuli za wiki hii huko Kitui ikizingatiwa kwamba bado kipindi cha maombolezi ya kitaifa kwa ajili ya Raila kinaendelea.

Website |  + posts
Share This Article