Rais William Ruto amemteua Douglas Kanja kuwa Inspekta Mkuu wa Polisi.
Kanja kwa sasa anakaimu wadhifa huo kufuatia kujiuzulu kwa Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome siku chache zilizopita.
Sasa anasubiriwa kupigiwa msasa na bunge la kitaifa na lile la seneti kabla ya kuteuliwa rasmi kwa wadhifa huo ikiwa uteuzi wake utaidhinishwa na mabunge yote mawili.
“Inspekta Mkuu mteule amepata mafunzo ya wigo mpana ya usalama kutoka ndani na nje ya nchi,” alisema Rais Ruto kupitia taarifa iliyotiwa saini na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.
Kanja alijiunga na huduma ya polisi mnamo mwaka 1985 na amepanda ngazi hadi kuhudumu kama kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi baada ya kujiuzulu kwa Koome siku chache zilizopita.
Huku mchakato wa Kanja kupigiwa msasa ukisubiriwa, Rais Ruto amemteua Gilbert Masengeli kuwa kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi.
Masengeli ameteuliwa na Rais Ruto kuwa Naibu Inspekta Mkuu wa Huduma ya Polisi wa Utawala.
Kwa upande mwingine, Eliud Kipkoech Lagat ameteuliwa kuwa Naibu Inspekta Mkuu wa Huduma ya Polisi nchini.