Rais William Ruto amempongeza Rais wa Rwanda Paul Kagame, kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa Urais ulioandaliwa Jumatatu.
“Kwa niaba ya raia na serikali ya Kenya, nakupongeza kwa kuchaguliwa tena kuhudumu muhula mwingine kama Rais wa jamuhuri ya Rwanda,” alisema Rais Ruto.
Ruto alimtakia Rais huyo heri njema anapoanza muhula mwingine uongozini, akielezea matumaini kuwa Rwanda itaendelea kuafikia maendeleo makubwa chini ya himaya yake.
“Tunasherehekea pamoja nawe chaguo la raia wa Rwanda na tunakutakia mafanikio unapoendelea kuongoza nchi hiyo kupitia amani, uthabiti na ustawi,” aliongeza Rais Ruto.
Kiongozi huyo wa taifa alitoa ahadi kwa Rais Kagame kwamba Kenya itaendelea kushirikiana kwa karibu na Rwanda kwa manufaa ya raia wa nchi hizo mbili.
“Natazamia kuendelea kushirikiana na wewe katika maswala ya kanda hii na Afrika kwa jumla katika kuimarisha uhusiano wa raia wa Rwanda na Kenya,” alisema Rais Ruto.