Rais Ruto ampigia debe Raila Odinga anaposaka uenyekiti wa AUC

Marion Bosire
1 Min Read

Kiongozi wa taifa Rais William Ruto anaendelea kumpigia debe Raila Odinga mwaniaji wa Kenya wa wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika AUC.

Akizungumza huko Kakamega jana Jumamosi, Ruto aliwataka wakenya wamuunge mkono Odinga anapotafuta wadhifa huo kwani anatosha na ana ujuzi unaohitajika kuhudumu.

Ruto alihimiza wakenya waungane kwani sasa Kenya ina fursa ya kutoa mwenyekiti wa AUC uchaguzi utakapoandaliwa Februari mwakani.

Alifafanua kwamba wadhifa huo sio wa mtu binafsi bali ni wa nchi kwa jumla, na hivyo ni lazima wakenya wote wamuunge mkono waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.

Rais Ruto alikuwa akizungumza wakati wa hafla ya makaribisho nyumbani ya Wycliffe Oparanya tangu kuteuliwa kuwa waziri ambapo alisema azma ya Odinga ni fursa kwa Kenya kuhudumu katika kiwango mihimu.

Alitumia fursa hiyo pia kuhimiza umoja kati ya viongozi kwa ajili ya ufanisi wa taifa hili.

Kampeni ya Odinga ya wadhifa huo wa AUC imeshika moto sasa anapotafuta kuchukua mahala pa Moussa Faki Mahamat ambaye muda wake wa kuhudumu kama mwenyekiti wa AUC unafikia kikomo.

Rais Ruto anatarajiwa kuzindua rasmi uwaniaji wa Raila Odinga wa wadhifa huo Jumanne Agosti 27, 2024.

Share This Article