Rais William Ruto amealika Kazakhstan kuifanya Kenya na bandari ya Mombasa kuwa kitovu cha usafirishaji wa nafaka katika kanda hii.
Wakati wa mkutano na Rais wa Kazakhstan, Kassym Jomart Tokayev pembezoni mwa mikutano ya baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini New York Marekani, Rais Ruto alisema Kenya na Kazakhstan pia zinachunguza kwa pamoja maswala ya manufaa kwa raia wake kwa lengo la kuendeleza ushirikiano katika biashara na uwekezaji, uvumbuzi wa sayansi na teknolojia, utosheleshaji wa chakula na uhamaji wa wafanyakazi.
Wakati huo huo, Kenya inaimarisha uhusiano baina yake na Ureno ili kufungua fursa katika maswala yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Katika taarifa yake baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Ureno, Marcelo Rebelo de Sousa, Rais Ruto alisema msaada wa kiufundi wa Ureno utaimarisha sekta ya nguo, mashine na vifaa nchini na uongezaji thamani kwa mazao ya kilimo. Alisema hatua hiyo itazalisha utajiri kwa raia wa mataifa yote mawili.