Rais William Ruto amesema atachukua hatua mwafaka, kuhusu maswala mbali mbali yaliyoibuliwa na wakenya, ikiwa ni pamoja na mienendo ya baadhi ya viongozi na maafisa wa serikali.
Akizungumza leo Ijumaa aliposhiriki mazungumzo na vijana kupitia mtandao wa X, kiongozi wa taifa alisema mara kadhaa alilazimika kuzungumza na baadhi ya viongozi hao kuhusu mienendo yao.
“Nimekuwa na kikao na Karen Nyamu kama mzazi na kumshauri abadili mambo kadhaa…..kuhusu kiburi, sio kila mtu huelewa mbinu za mawasiliano. wakati mwingi sisi husema mambo ambayo hatuyamaanishi,” alisema Rais Ruto.
Rais pia alisema atachukua hatua mwafaka dhidi ya maafisa wafisadi serikalini.
“Iwapo kuna madai ambayo yamethibitishwa dhidi ya waziri yeyote au afisa yeyote wa serikali na kufikishwa mahakamani, nitawafuta kazi, sitasubiri mchakato wa mahakama kukamilika,” alisema kiongozi wa taifa.
Wakati huo huo Rais Ruto alisema anakusudia kumteua mshauri wa maswala ya vijana kuangazia mambo yanayowaathiri vijana.
Katika mazungumzo hayo na vijana, Rais alidokeza kuwa mwaka jana vijana 120,000 walienda kufanya kazi katika mataifa ya nje.
“Tunatia saini mikataba 19 ya maelewano kuhusu ajira, ili kutoa fursa zaidi kwa wakenya kufanya kazi ughaibuni,” alisema Rais Ruto.
Kwa mujibu wa Rais, juma lijalo wataalam 36,000 katika sekta ya ujenzi wataajiriwa, huku tangazo la nafasi za kazi likitolewa hivi karibuni.