Rais William Ruto leo Jumatano amekutana na viongozi wa kidini katika Ikulu ya Nairobi.
Viongozi hao walikuwa wa kutoka makanisa ya Kievanjilisti na Pentekoste, wakiongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa la Redeemed Gospel Kepha Omae.
Wakati wa mkutano huo, Rais Ruto ameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi hao katika kuhakikisha uwiano wa kitaifa.
“Viongozi wa kidini na wa serikali wanawatumikia watu wale wale na daima wamefanya kazi pamoja kuhakikisha uwiano wa kitaifa na kutoa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na elimu, afya na kuwasaidia watu wasiojiweza,” alisema Rais Ruto.
“Tunaahidi kudumisha ushirikiano huu.”
Mkutano huo unakuja siku chache baada ya viongozi wa kidini humu nchini kushutumu uongozi wa serikali ya Kenya Kwanza.
Maaskofu wa Kanisa Katoliki ndio waliokuwa wa kwanza kuibua shutuma dhidi ya serikali ya Rais Ruto waliyosema imetepetea kazini.
Walitaja mambo kadha wa kadha ikiwemo gharama ya juu ya maisha, ushuru wa kiwango cha juu wanaotozwa Wakenya, Bima ya Afya ya Jamii, SHIF na mpango wa nyumba za gharama nafuu wakiyataja kuwa mwiba kwa Wakenya wengi.
Isitoshe, baadhi ya viongozi wa makanisa wamekataa michango ya fedha iliyotolewa na Rais.
Rais Ruto anafahamika kwa kutoa michango ya fedha kufadhili shughuli za makanisa nchini.