Rais Ruto akutana na viongozi wa chama cha ANC

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto aliandaa kikao na viongozi wa chama cha Amani National Congress, ANC cha Waziri aliye na Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi katika Ikulu ya Nairobi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais alisema kwamba vyama thabiti vya kisiasa ni msingi mzuri wa umoja wa kitaifa na utawala wa kidemokrasia wenye nguvu.

“Ili kuunganisha jukumu lao katika demokrasia, vyama vya kisiasa ni lazima vikome kuwa tu vyombo vya uchaguzi na kuwa vyombo vya kuhimiza mshikamano wa kitaifa na mabadiliko,” alisema Rais Ruto.

Kulingana na Mudavadi, kikao hicho kilisisitiza kujitolea kwao kuimarisha miungano ya kisiasana kuhakikisha kuimarika kwa uchumi.

“Kupitia mazungumzo muhimu, tunaunda njia ya mabadiliko ya kuafikia ufanisi siku za usoni kwa wakenya wote, tukitoa kipaumbele kwa ushirikiano na maono ya kimkakati katika kila hatua.” alisema Mudavadi.

Waliohudhuria mkutano huo wa leo ni pamoja na kiongozi wa chama cha ANC Issa Timamy ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Lamu, katibu mkuu wa chama Omboko Milemba ambaye pia ni mbunge wa Emuhaya na mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Kelvin Lunani.

Wengine ni Waziri aliye na Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, mwenyekiti wa chama cha UDA Cecily Mbarire, katibu mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malala na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah kati ya wengine wengi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *