Rais Ruto akubaliana na Odinga kuhusu kustawisha ugatuzi

Rais alisema hatua hiyo itahakikisha maendeleo katika sehemu zote za nchi.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amemsifia aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kwa kuunga mkono serikali akisema uamuzi wa kushirikiana naye serikalini umetoa uthabiti unaohitajika.

Kiongozi wa nchi alisema hayo huko Ndori kaunti ya Siaya, katika hafla ya mazishi ya aliyekuwa mlinzi wa kibinafsi wa Raila George Oduor.

Kulingana na Ruto utulivu unaoshuhudiwa serikalini umesababisha uchumi uwe dhabiti na ukue.

Rais aliahidi shilingi milioni 20 zitakazotumiwa kukarabati shule ya upili ya Ramba kwa heshima ya mwendazake George Oduor.

Kuhusu ugatuzi, kiongozi wa nchi alikubaliana na Odinga kuhusu haja ya kuustawisha na kuhakikisha maendeleo katika sehemu zote za nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Raila Odinga aliwataka wabunge kuachia magavana utekelezaji wa mipango mbali mbali na kuangazia jukumu lao kuu la uangalizi.

Raila salisema magavana wanastahili kupatiwa muda wa kutekeleza mipango ya maendeleo huku mgao zaidi wa pesa ukitolewa na serikali kuu kwa kaunti ili kuafikia malengo ya ugatuzi.

Aliambia wabunge wakubalie serikali kuu ielekeze pesa za hazina ya kitaifa ya maendeleo ya maeneo bunge NG-CDF kwa serikali za kaunti kama sehemu ya pesa zinazohitajika za maendeleo.

Wakati huo huo Raila Odinga, alipendekeza kuvunjiliwa mbali kwa mashirika mawili makuu ya serikali yanayohusika na ujenzi wa barabara akisema hayana umuhimu tena wakati huu ambapo usimamizi wa barabara umegatuliwa.

Raila alitaja shirika la kitaifa la barabara za maeneo ya mashinani – KeRRA na lile la barabara za mijini – KURA akisema yanafaa kuvunjiliwa mbali na pesa zinazoelekezwa huko zitolewe kwa kaunti.

Raila alimsifia marehemu Oduoro akisema alikuwa afisa bora wa ulinzi ambaye alipokea mafunzo nchini Afrika Kusini, Israel na Marekani, aliongeza kusema kwamba inauma kupoteza msiri wake miaka kumi baada ya kupoteza mwanawe Fidel Odinga.

Website |  + posts
Share This Article