Rais William Ruto amekariri kujitolea kwa serikali yake kuhakikisha inafuata sheria, kulinda katiba na kujitolea kwake kuhakikisha mauaji ya kiholela na utekaji nyara vinasitishwa.
Akizungumza katika hafla ya mazishi ya mama ya Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula katika kaunti ya Bungoma, Rais alisema kwamba tayari amehakikisha uhuru wa huduma ya taifa ya polisi.
Kutokana na hilo anatarajia uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu visa vya utekaji nyara nchini na yeyote atakayepatikana na hatia akabiliwe kwa mujibu wa sheria.
Rais Ruto alionya pia viongozi dhidi ya siasa za migawanyiko zinazolenga kuchochea na kuhujumu ajenda ya serikali ya maendeleo.
Onyo jingine alilotoa ni kwa vijana nchini akiwataka wakome kutumia vibaya mitandao ya kijamii kwani wanajiweka katika hatari ya kushtakiwa kulingana na sheria ya mwaka 2018 ya matumizi mabaya ya kompyuta na makosa ya kimtandao.
Anataka udhibiti uwepo katika kufurahikia haki mbali mbali humu nchini huku akiomba viongozi na wakenya kwa jumla kuwa makini na picha wanayoonyesha wawekezaji wa kimataifa.
Mazishi hayo ya Mama Anne Nanyama Wetang’ula, yanahudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi, spika wa bunge la seneti Amason Kingi na wabunge kadhaa wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah na kiongozi wa wachache Junet Mohamed.
Magavana kadhaa pia walihudhuria akiwemo wa Trans Nzoia George Natembeya, Ken Lusaka wa Bungoma na Paul Otuoma wa Busia.