Rais William Ruto ametangaza nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wote wa umma kuanzia tarehe moja mwezi Julai mwaka huu.
Kiongozi wa taifa alisema serikali imeidhinisha nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wa umma kutokana na nyakati ngumu za kiuchumi.
Aidha alisema uamuzi huo unaendana na mapendekezo ya tume ya uratibu wa mishahara humu nchini huku wafanyakazi wa viwango vyote wakitarajiwa kupokea kati ya asilimia saba na 10 ya nyongeza hiyo.
Akizungumza siku ya Ijumaa alipozindua huduma za serikali mtandaoni, Rais Ruto alisimamisha nyongeza ya mishahara ya Rais, naibu Rais, Jaji Mkuu na mawaziri, iliyopendekezwa na tume ya uratibu wa mishahara na marupurupu SRC.
‘Ninafahamu kuna pendekezo la tume ya SRC kuongeza mishahara ya baadhi ya watumishi wa umma. Kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi, tumeidhinisha nyongeza ya mishahara ya watumishi wa umma kuanzia kesho,” alisema Rais Ruto.