Rais Ruto ahimiza umoja kati ya Wakenya

radiotaifa
1 Min Read

Rais William Ruto amehimiza Wakenya wawe na umoja huku akilitaka kanisa kuendelea kuhubiri amani.

Akizungumza katika ibada ya pamoja huko Kipsitet kaunti ya Kericho, Rais alishukuru wakazi wa eneo hilo kwa kupigia kura chama cha UDA na kuahidi kwamba serikali itakamilisha mradi uliopendekezwa wa uwanja wa ndege.

Kiongozi wa nchi alisema mradi huo, utahakikisha kwamba kaunti ya Kericho inafanya biashara ya kimataifa kwani uchukuzi wa bidhaa utarahisishwa.

Kulingana na Rais miradi iliyokwama ya barabara katika kaunti hiyo pia itakamilishwa kwani sasa kuna fedha za kutosha za kuifadhili.

Rais vile vile alihimiza viongozi kutupilia mbali tofauti zao na kuhudumia wakenya, kwani tofauti zitalemaza maendeleo.

Viongozi wa kidini na wa kisiasa alisema wanahudumia wakenya wale wale na hivyo wanastahili kushirikiana.

Kuhusu kutoa michango kanisani, kiongozi wa nchi alisema hatakoma kwani anafahamu umuhimu wa kutoa. Alisema pia kwamba yeye hujitolea kutoka moyoni anapotoa michango kama hiyo.

Matamshi yake yanafuatia hatua ya uongozi wa kanisa katoliki jimbo la Nairobi ya kukataa michango ambayo Rais alitoa katika kanisa katoliki la Soweto, Kayole kaunti ya Nairobi.

Mchango huo ulitolewa siku chache baada ya baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini, kumulika serikali kwa kutoshughulikia changamoto za wananchi.

Share This Article