Rais William Ruto amefanya mkutano na viongozi wa kike leo kutokana na kuongezeka kwa mauaji ya wanawake humu nchini.
Huku akiangazia ukweli kwamba wanne kati ya kila wanawake watano wanaouawa wanapoteza maisha kutokana na vurugu za kimapenzi, Rais alisisitiza haja ya hatua za haraka katika kulinda haki na heshima ya wanawake na wasichana.
Katika mkutano huo Rais Ruto alitoa salamu za pole kwa wote ambao wameathiriwa na vurugu za aina hiyo huku akipongeza viongozi wa kike kwa kujitolea kupendekeza sukuhisho.
“Kulinda mabinti, dada na mama zetu kunaanza nyumbani, katika jamii zetu na kupitia kwa taasisi mbali mbali.” alisema Rais Ruto.
Serikali inapanga kuimarisha madawati ya kushughulikia masuala ya kijinsia katika vituo vya polisi na kuzindua huduma sawia katika hospitali za umma ili waathiriwa wapate usaidizi haraka.
Rais aliagiza pia wahusika katika idara ya haki ya jinai kushughulikia kesi hizo haraka na kuwajibisha watekelezaji.
Kama sehemu ya mpango mpana, serikali inazindua kampeni ya “Safe Homes, Safe Spaces” yaani nyumba salama, maeneo salama, wakati wa maadhimisho ya siku 16 za uanaharakati wa kupinga dhuluma za kijinsia.
Maadhimisho hayo yanaanza Novemba 25 na tayari shughuli hiyo imetengewa shilingi milioni 100. Kampeni hii inalenga kuhamasisha na kutoa raslimali muhimu kwa waathiriwa kama vile nambari za simu zisizotozwa malipo na ushauri nasaha.
Rais Ruto vile vile aliwaomba viongozi wa dini, wazazi na mashirika ya kijamii kukuza maono chanya kuhusu haki za wanawake akisema kwamba “Haki za wanawake ni haki za binadamu pia.”
Kiongozi wa nchi alihimiza ushirikiano wa sekta zote za jamii katika kukabiliana na mauaji ya wanawake na kubuni mazingira salama kwa wanawake na watoto.
Taifa linapojiandaa kwa kampeni hiyo,Rais Ruto anaomba kila mkenya kujiunga na vita dhidi ya uovu huo kwani, “Tukiungana kama taifa, tutatokomeza janga hili.”.