Rais Ruto afungua kituo cha afya kwa maafisa wa GSU

Huduma ya Taifa ya Polisi pia inatarajiwa kupanua huduma za matibabu ya akili, kuwasaidia maafisa wa polisi wanaoathiriwa na hali hiyo.

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto afungua kituo cha afya kwa maafisa wa GSU.

Rais William Ruto leo Ijumaa amefungua kituo cha afya kwa maafisa wa General Service Unit (GSU) katika chuo cha mafunzo ya polisi cha Embakasi B jijini Nairobi.

Kituo hicho, kinacholenga kuimarisha utoaji huduma za afya kwa maafisa hao na familia zao, kilizinduliwa wakati wa sherehe za 50 za kufuzu kwa makurutu wa GSU.

Akizungumza alipoongoza sherehe hizo, Rais Ruto alisema kupitia bima ya Usalama Cover inayohudumu ndani ya Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA, zaidi ya maafisa 138,000 wa polisi na wale wa magereza pamoja na familia zao, sasa watapata huduma bora za afya zilizoimarishwa.

Bima hiyo inashughuliki wagonjwa wa kulazwa, wale wa kutibiwa na kurejea nyumbani, upasuaji, huduma za kina mama kujifungua, matibabu ya kitaalam, matibabu ya meno, macho na huduma za uchunguzi wa kimatibabu.

“Maafisa wanaweza kutafuta huduma za matibabu katika vituo mbalimbali vya afya kote nchini, huku uidhinishaji wa kidijitali ukichukua chini ya dakika 15,” alisema Rais Ruto.

Huduma ya Taifa ya Polisi pia inatarajiwa kupanua huduma za matibabu ya akili, kuwasaidia maafisa wa polisi wanaoathiriwa na hali hiyo.

Share This Article