Maafisa wa Polisi nchini Nigeria, wanachunguza vifo vya wachimbaji madini 37 waliokuwa wakizuiliwa kwenye korokoro za polisi.
Kulingana na utawala nchini humo, watu hao waliokuwa wamekamatwa kwa madai ya uchimbaji haramu wa madini, walifariki kutokana na kuzuka kwa ugonjwa ndani ya korokoro hizo, lakini ripoti zingine zinaashiria walifariki baada ya kukosa hewa ya kutosha.
Msemaji wa idara ya usalama na ulinzi Seberu Siyaka, alisema kuzuka kwa ugonjwa huenda kulisababisha maafa hayo, huku miili hiyo ikifanyiwa uchunguzi kubainisha chanzo cha vifo hivyo.
Hata hivyo, Siyaka hakutaja ugonjwa huo unaoshukiwa kusababisha vifo hivyo.
Manusura mmoja Dauda Shehu, aliwaambia wanahabari kuwa wafungwa 65 walikuwa wakizuiliwa kwenye kororkoro hilo ambalo halikuwa na hewa ya kutosha, na kuashiria huenda waliofariki hawakuwa na hewa ya kutosha.
“Tulikuwa tumejaa kupita kiasi, na hatukuweza kupumua vizuri,” alisema Shehu.