Rais Ruto afanya ziara rasmi nchini Marekani

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto

Rais William Ruto aliondoka hapa nchini Jumatano jioni kuelekea nchini Marekani, kwa ziara rasmi ya kiserikali.

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, ziara ya Rais Ruto inaashiria kujitolea kwa Kenya katika uvumbuzi wa teknolojia na jukumu lake muhimu kama mshirika wa kibiashara na Marekani.

Rais Ruto anatarajiwa kuzuru bonde la Silicon katika eneo la San Francisco, ambapo atakutana na viongozi wa Microsoft, Intel, Google na Apple, miongoni mwa wengine.

Aidha ziara hiyo inalenga kuimarisha fursa za uwekezaji na uhusiano wa kibiashara hasaa katika kukuza sekta ya biashara zinazochipuza almaarufu  “Silicon Savannah.”

Baadaye kiongozi wa taifa atahudhuria mkutano wa 78 wa Umoja wa Mataifa Jijini New York.

“Mkutano huo utatathmini ajenda ya maendeleo ya mwaka 2030, pia utashughulikia changamoto zinazoghubika dunia kama vile janga la mabadiliko ya tabia nchi pamoja na madeni,”alisema Mohamed.

Pembezoni mwa mkutano huo wa umoja wa Mataifa, rais Ruto pia ataongoza mkutano wa kamati ya viongozi wa nchi na serikali wa bara Afrika kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na kushiriki majadiliano kuhusu uchumi wa baharini.

Share This Article