Rais Ruto aelekea Marekani kuhudhuria mkutano wa UNGA

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto aelekea Marekani kuhudhuria mkutano wa UNGA.

Rais William Ruto Ijumaa usiku aliondoka hapa nchini kuelekea Jijini New York, Marekani, kuhudhuria makala ya  79 ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa-UNGA. 

Mkutano huo wa kimataifa huwaleta pamoja viongozi wa dunia kushughulikia maswala muhimu ya kimataifa, huku mkutano wa mwaka huu ukiangazia maendeleo endelevu, uongozi mwafaka duniani na hatua za kukabiliana na tabia nchi.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed, alisema Rais Ruto atapigia debe mabadiliko katika taasisi za kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa, kuhakikisha zinavifaa vinavyohitajika kukabiliana na changamoto zilizopo.

Kulingana na Hussein, kiongozi wa taifa atashiriki mazungumzo ya ngazi za juu kuhusu kuziba pengo katika sekta ya dijitali na kuunga mkono ujumuishaji katika uchumi wa dijitali.

Aidha mazungumzo hayo pia yataangazia teknolojia ibuka kama vile akili mnemba AI na usimamizi wa deta kuhakikisha zinasimamiwa kwa usawa.

Katika mkutano huo pia, Rais atashinikiza kuongezwa kwa uwakilishi wa Afrika katika taasisi za kimataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Taasisi ya fedha duniani IMF.

Website |  + posts
Share This Article