Rais Ruto abuni jopokazi la kubaini fedha inazodaiwa Kenya

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto amebuni jopokazi ambalo limekabidhiwa jukumu la kubaini ni kiasi gani cha fedha ambazo nchi hii inadaiwa. 

Kumekuwa na taarifa ambazo hazijathibitishwa zinazoashiria kwamba deni la taifa kwa sasa ni takriban trilioni 10.

Rais William Ruto katika hotuba yake kwa taifa kutoka Ikulu ya Nairobi leo Ijumaa amesema jopokazi hilo lina muda wa miezi mitatu kufanya uchunguzi wa kisayansi na kutegua kitendawili cha deni la taifa ni la kitita cha pesa ngapi.

“Ukaguzi huu utawapatia Wakenya ukweli wa mambo kuhusiana na kiwango na hali ya deni hilo, namna rasilimali za umma zilivyotumiwa, na litatoa mapendekezo ya kusimamia deni letu la taifa katika njia ambayo ni endelevu na katika usawa kizazi hadi kizazi,” alisema Rais Ruto.

Kiwango cha fedha ambazo nchi hii inadaiwa, ndani na nje ya nchi, kimekuwa suala tete ambalo limelezua maoni mbalimbali miongoni mwa viongozi humu nchini wakati mabilioni ya fedha yakitumiwa kulipa deni hilo.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah ni miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa wakishinikiza deni la taifa kutangaziwa Wakenya hadharani.

Omtatah anahisi kuwa huenda fedha za umma zinabadhiriwa katika kulipa deni hilo ambalo kima chake hakijulikani bayana.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *